Wednesday, September 3, 2014

Jide: Maadui zangu wamebadilisha wimbo

Malkia wa muziki wa R&B, Lady Jay Dee
Dar es Salaam. Malkia wa muziki wa R&B, Lady Jay Dee amedai kuwa maadui zake wamebuni njia mpya ya kumwangusha, baada ya zile za awali kutofanikiwa.
Katika waraka mrefu aliouandika katika mtandao wa facebook, Lady Jay Dee alisema watu wasiopenda mafanikio yake wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kumwangusha, lakini hata hivyo wameshindwa.
Jay Dee analalamikia habari iliyoandikwa juu yake kuwa amekuwa katika uhusiano mpya na kijana aliyemzidi umri, jambo analosema halina ukweli.
Habari hiyo inahusishwa na kile kilichodaiwa kuwa mwanamuziki huyo ameachana na mume wake, Gadner G Habash, ambaye ni mtangazaji wa kituo cha redio Times FM.
Jide ameandika: “Hata kama nimeachana na mume wangu, siyo sababu ya kunihusisha katika uhusiano na mwanamume mwingine yeyote. Habari hii imenivunjia heshima. Nafikiri lengo la uzushi huu ni kumfanya Lady Jaydee aonekane mtu asiyefaa.”
Habari hiyo ilipambwa na picha ambazo alizipiga mwenyewe kwa kutumia simu ya mume wake.
Aliongeza: “Ni vizuri kuzusha vitu ambavyo angalau unavijua, hizi picha zilipigwa kwa simu ya Gadner ambaye mnasema nimeachana naye, hamuoni kama mnawadanganya watu?”
Aliongeza kuwa huenda aliyeanzisha habari hizo ameona zile ambazo zilikuwa zikivuma wakati fulani, zimeshuka chati.
Alihoji: “Je, wimbo Jay Dee mgumba, Jay Dee tasa umeshuka chati ndiyo maana mmeamua kuleta mwingine?”
Hata hivyo, alisema lengo la wanaoanzisha uzushi juu yake ni kumdhoofisha lakini anaamini jinsi alivyoshinda vita ya kwanza, atashinda tena vita ya pili. “Hata kama ndoa yangu haiko sawa, niacheni.
Lakini isiwe sababu ya kuendelea kunichafua kwa maneno ya kizushi. Siyo lazima niandikwe, kwa sababu nilikuwapo kabla ya kuandikwa sana... nitaendelea kuwapo bila kuandikwa.”

Hofu ya Borno kutekwa na Boko Haram


Wanamgambo wa Boko Haram wanatumia silaha nzito kama hizi kupambana na jeshi     

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan anafanya kikao cha dharura cha ulinzi mjini Abuja huku ripoti zikisema kuwa huenda jimbo lililo Kaskazini mashariki la Borno likaingia mikononi mwa kundi la wanamgambo wa Boko Haram.
Vyombo vya habari vinasema kuwa viongozi saba wa kitamaduni wametoroka makwao.
Siku ya jumamne kundi la Boko Haram liliuthibiti mji wa Bama ambao ni mji wa pili kwa ukubwa kwenye jimbo la Borno ambapo liwaua watu wengi na kuwalazimu maelfu ya wengine kukimbia makwao .
Kwa sasa ni mji mkuu tu wa jimbo la Borno wa Maduguri ulio chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali.